KWANINI MIMI NINAABUDU SIKU YA
JUMAPILI?
Baada ya
kusoma majadiliano mengi kwenye mitandao ya kijamii kuhusu malumbano ya siku
gani ni halali ya kusali katika Biblia, kwamba ni Jumapili au Jumamosi; Kwa
faida ya wasomaji wangu katika ukurasa huu ambao wamekuwa wakiomba nitoe maoni
kuhusu ipi siku ni halali, leo nimeona kujibu maombi yao kwa kuwasilisha makala
haya huku nikitoa sababu zangu 5 kama hizi zifuatazo:
I.YESU
KRISTO ALIFUFUKA SIKU YA JUMAPILI
Katika
historia ya kibiblia; tendo la Yesu kufufuka siku ya Jumapili lilifungua
ukurasa mpya wa Agano Jipya. Maandiko ya Injili yanathibitisha ya kwamba Yesu
alifufuka siku ya kwanza ya juma, ambayo ni Jumapili. (Mk 16:9; Lk 24:1,13,21)
Pamoja na
kwamba kifo cha Yesu ndicho kilitengeneza wokovu wetu, lakini kufufuka kwa Yesu
ndiko kunakotupa nguvu za kushangilia na kuabudu kwa shangwe. Ibada iliyo hai
imejengwa juu ya kufufuka kwa Yesu Kristo.
II.YESU
ALIWASILISHA MBINGUNI DHABIHU YA DAMU YAKE SIKU YA JUMAPILI
Tukio
jingine la kihistoria ambalo lilibadilisha mfumo mzima wa kiibada ni pale
ambapo Yesu alisema anapaa kwenda kwa Baba na Mungu wake.
Yesu
alipomtaja Baba kwa jina la Mungu alisema hivyo akiwa ndiye Kuhani mkuu mpya wa
Agano Jipya ambaye alitakiwa kupeleka damu yake mwenyewe kwenye Kiti cha Rehema
mbinguni ili kukamilisha dhabihu ya Agano jipya.
Yesu
alisema maneno haya baada ya kumkatalia Mariamu asimguse kwanza mpaka atimilize
zoezi ya kuwasilisha dhahibu ya damu yake mbele za Mungu Baba yake:
“Yesu
akamwambia, usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa
ndugu zangu ukawambie ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, na Mungu
wangu naye ni Mungu wenu.” (YH.20:17)
Sasa siku
ambayo Yesu aliifanya kazi hii ilikuwa ni Jumapili baada ya kufufuka kutoka
katika wafu. Najuaje kwamba aliwasilisha dhahibu mbinguni siku ya Jumapili?
Ushahidi wangu ni pale ambapo maandiko yenyewe yamekiri ya kwamba Yesu alipaa
mbinguni siku ile ile kwenda mbinguni; na kwamba alishuka dunia ile ile jumapili; na kuwatokea
wanafunzi siku ile ile ya kwanza ya juma:
“Ikawa
jioni, siku ile ya siku ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango
imefungwa kwa sababu ya hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati,
akawaambia amani iwe kwenu.” (YH.20:19)
III.ROHO
MTAKATIFU ALISHUKA DUNIANI JUMAPILI
Tukio la
tatu la kihistoria katika mambo ya kiibada kwa mujibu wa Agabno Jipya ni ujio
wa Roho Mtakatifu duniani. Kutimia kwa ahadi ya Roho Mtakatifu siku ya Jumapili
kuliifungua siku hiyo kuwa ibada ya
kwanza ya kuabudu Mungu katika roho na kweli kama Yesu alivyomtabiria mwanamke
Msamaria kisimani (MDO.2:1-4)
“Lakini
saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho
na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.” (YH.4:23)
Unaona?
Huu ulikuwa ni mjadala wa mahali panapostahili kuabudia kama ni Hekaluni
Yerusalemu au juu ya mlima wa Samaria. Yesu akatabiri za kuja kwa mabadiliko ya
mtindo wa kuabudu, mazingira ya kuabudia na siku ya kuabudu. Siku ya ujio wa
Roho Mtakatifu ambayo ni Jumapili ndipo mabadiliko ya kiibada yalifanyika kwa
mara ya kwanza.
IV. KANISA LA
KRISTO LILIZALIWA SIKU YA JUMAPILI
Huko nyuma
mwanza wa huduma za Yesu aliwahi kutabiri akimwambia Petro ya kwamba:
“Nami
nakwambia, wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; na
milango ya kuzimu haitalishinda.” (MT.16:18)
Kibiblia
tunafahamu ya kwamba kanisa hili lilizaliwa siku ya Pentekoste kwa sababu
injili ya kwanza ya mitume ilianza rasmi baada ya kumpokea Roho Mtakatifu kama
Yesu alivyokuwa ameagiza.
Ni baada
ya mitume na wakristo wengine jumla ya watu 120 walipojazwa Roho Mtakatifu na
kusema kwa lugha nyingine Petro alihubiri na wakatubu na kubatizwa waamini
wapya 3000. Hawa ndio mavuno ya kwanza yaliyozaa kanisa la kwanza.
Na mavuno
haya yalipatikana siku ya Jumapili. Kwa maana imeandikwa na: Na siku ile…… ipi?
Siku aliposhuka Roho Mtakatifu…. Siku gani? Jumapili!
V. KANISA LA
KRISTO LILIKUTANA KIIBADA SIKU YA JUMAPILI
Kama
ilivyo desturi, ibada yo yote inayo mambo au matendo ya kiibada ambayo
huitambulisha kuwa hiyo kweli ni ibada.
Kuna
matendo mawili ya kiibada ambayo tunasoma kanisa lilifanya siku ya Jumapili.
Tendo la kwanza ni Meza ya Bwana inaitwa siku ya kumega mkate (Mdo. 20:7)
Na tendo la pili ni matoleo ya changizo na
sadaka. Hakuna ubishi ya kwamba mojawapo ya tukio maarufu la kiibada ni
utoaji. Tunasoma ya kwamba kanisa la
kwanza likikutana kiibada na kufanya matoleo (1 Kor.16:1-2
Kwangu
miye, haya mambo makubwa, mazito ya kihistoria na kiibada ndiyo yananishawishi
niamini na kujua ya kwamba Ibada za Agano Jipya ni siku ya kwanza ya Juma
ambayo ndiyo jumapili.
Ndugu
msomaji wangu. Ukurasa huu ni kwa ajili ya kuelimishana na si mahali pa
malumbano na matusi.
Katika
makala haya sitarajii kufanya malumbano ya wapinzani wa siku ya jumapili. Ila
naomxa kutahadharisha mapema ya kwamba kama ukifanyika uchokozi wa aina yoyote
mabishano au matusi, safari Hii nitalazimika kujibu majibu ya ukweli mzito na
makali na hapo nisije kulaumiwa.
Kama
umesoma post hii na imekubariki basi nijulishe kwa ku-like na pia warushie
marafiki zako pia.
Silvester
Gamanywa
No comments:
Post a Comment