Thursday, February 15, 2018


ACHA KUKIMBIZANA NA"MANABII" ILI KUPATA "NENO KUTOKA KWA MUNGU" ANZA KUKIMBIZANA NA NENO THABITI ZAIDI LA KINABII.
Wapenzi nimesikia hili wazo likidondoka ndani yangu nilipokuwa najiandaa kulala na mara lilipodondoka nikaanza kutafakari jinsi watu wanavyokimbia huko huko ili eti "Kusikia neno toka kwa Bwana kwa ajili yao kupitia manabii."
Mimi binafsi nakubali kabisa kuwa manabii wapo hata leo ila nisichokubaliana nacho ni kwamba manabii wa Agano Jipya ni sawa na manabii wa Agano la Kale.

Katika Agano Jipya nabii ni mmojawapo kati ya zile huduma tano teule za Waefeso 4:11 na ni mojawapo ya huduma ongozi ndani ya kanisa sawa na na I Kor. 12: 28 na Matendo 13: 1 na pia mojawapo kati ya huduma mbili ziwekazo msingi wa kanisa sawasawa na Efeso 2: 20.
Nabii ni mfunuaji na mtafsiri wa siri na mafumbo ya Mungu kupitia kuhubiri na kufundisha kulikovuviwa.
Nabii huleta kwetu siri ya Ufunuo wa Kristo kupitia mahubiri na mafundisho.
Nabii anatuthibitisha katika kumjua Kristo kupitia mahubiri na mafundisho.
Huduma hii inavyofanya kazi katika Agano Jipya ni tofauti kabisa na ilivyokuwa inafanya kazi katika Agano la Kale.
Sababu kubwa ikiwa ni kwenye Agano Jipya kila amwaminiye ana uwezo wa kuisikia sauti Yake maana imeandikwa kondoo wangu waisikia sauti Yangu. Tena imeandikwa sehemu nyingine "hao rafiki Zako huisikia sauti yako" na Yesu anatuita sisi marafiki na sio watumwa kwa hiyo sote twaisikia sauti ya Mungu.

Pia Roho Mtakatifu anaifunua kwetu sauti ya Mungu maana anayatwaa yaliyo Yake na kuyafunua kwetu so mwamini hahitaji "Nabii" hapo anamhitaji Roho Mtakatifu.
Wakati kwenye Agano la Kale Bwana Mungu alikuwa hafanyi lolote pasipo kwanza kuwafunulia watumishi Wake manabii siri Zake katika Agano Jipya atakapokuja huyo Roho wa Kweli atatuongoza na kututia katika kweli yote na atatupasha moja kwa moja habari za mambo yajayo.
Agano la Kale Roho Mtakatifu alikuwa juu ya manabii, makuhani na Wafalme katika Agano Jipya yupo juu na ndani ya kila amwaminiye.

Nabii katika Agano Jipya ni mojawapo ya huduma tano teule ambaye hufanya kazi kwa kushirikiana na hizo huduma zingine ili kuukamilisha Mwili wa Kristo hata kazi ya huduma itendeke. Kwa mujibu wa Agano Jipya hamna kitu kama nabii aliye peke yake asiyeshirikiana na wenzake na ambaye badala ya kujenga Mwili wa Kristo anajenga jina lake na ufalme wake.

Nabii anahitaji kushirikiana na mitume, wainjilisti, wachunagaji na waalimu kuwakamilisha watakatifu hata kazi ya huduma itendeke na mwili wa Kristo Ujengwe. Huku akishirikiana na hizo huduma zingine atahakikisha sote tunafikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu na sio yeye nabii. Nabii wa kweli huliinua Jina la Yesu na sio la kwake. Humhubiri Kristo na sio yeye. Huutafuta Utukufu wa Kristo na sio wake.

Watoto wa Mungu wanahitaji kujua kuwa Mungu anatamani kujifunua kwao na kuzungumza nao kupitia neno Lake. Maana Mungu na Neno Lake ni Wamoja.
Mungu anataka tulisome neno Lake ili alifunue kwetu na tusikie sauti Yake na sio kukimbizana na manabi, matokeo yake tukaparamiana na manabii wa uwongo wanautupa maunabii ya uwongo na kututoza kila aina ya sadaka hatarishi kwa kazi ya Msalaba wa Yesu.
Mtu wa Mungu embu tubadilike na tuanze kuwa na kiu ya kweli na sio mbwembwe.
Tafakari niliyoandika na Bwana akakupe ufahamu katika mambo yote.

No comments:

Post a Comment