Thursday, June 23, 2016



*BWANA akamwambia Abramu, alipokwisha kutengana na Lutu, Inua sasa macho yako, ukatazame kutoka hapo ulipo, upande wa kaskazini, na wa kusini na wa mashariki na wa magharibi; maana nchi hii yote uionayo, nitakupa wewe na uzao wako hata milele. (MWA. 13:14-15 SUV).*
Kama vile Bwana alivyoongea na Abramu akamwambia ainue macho yake kutoka hapo alipo atazame kutoka hapo alipo upande wa kaskazini, na wa kusini, na wa mashariki na wa magharibi maana nchi yote aionayo atampa yeye n...a uzao wake hata milele, ni dhahiri tunaiona kanuni ya ajabu sana ya Mungu hapa.
Ibrahimu alikuwa amesimama katika nchi ya ahadi.
Akaambiwa ainue macho yake atazame pande zote.
Ni sehemu tu ya ile nchi ambayo aliweza kuiona ndiyo angepewa.
Bibilia ni kama nchi ya ahadi kwetu maana ndani yake kumejaa ahadi za Mungu kwa ajili yetu lakini haziwi zetu kwa sababu zimeandikwa bali zinakuwa zetu kwa sababu tunajua kuwa zimeandikwa na tunaachilia imani zetu kuzipokea.
Usipokuwa msomaji wa neno huwezi kujua nini kimeandikwa na usipojua nini kimeandikwa huwezi kumwamini Mungu kwa hiyo ahadi na usipomwamini hutaiona hiyo ahadi ikitimia maishani mwako.
Naamini kaskazini ni kitabu cha Mwanzo, kusini ni kitabu cha Malaki, mashariki ni kitabu cha Mathayo na magharibi ni kitabu cha Ufunuo.
Soma bibilia Mwanzo hadi Malaki, Mathayo hadi Ufunuo, kila ahadi utakayoiona Mungu atakupa wewe na uzao wako.
Utakachofanikiwa kukiona kwa habari ya ahadi za Mungu humo kwenye maandiko ndo hicho Mungu atakupa katika maisha yako maana ahadi za Mungu zinarithiwa kwa imani na uvumilivu sasa huwezi kumwamini Mungu kwa kitu ambacho hata hujui kama kipo.
Bibilia ni kitabu cha ahadi na maagizo.
Wengi tunaishi chini ya kiwango kwa sababu hatujui.
Hatujaona.
Na hatujaona kwa kuwa hatujaamua kuinua macho yetu kusoma.
Soma bibilia hapo ulipo uzijue ahadi za Mungu maana Mungu analiangalia neno Lake apate kulitimiza.
Haliangalii lililoandikwa alitimize bali lile lililoandikwa ambalo wewe unalijua alitimize maana ukishalijua ni rahisi kumwamini Mungu kwa ajili ya hilo.
Acha uvivu.
Soma.
Mungu amezikuza ahadi Zake juu ya Jina Lake lote.
Soma ujue ahadi za Mungu maana ni zile tu unazojua ndizo zinamfanya Mungu azitimize.
Imani yako itasababisha Mungu kutimiza ahadi Yake maishani mwako.

No comments:

Post a Comment