Sunday, March 18, 2018

MAMBO 12 YANAYOWEZA KUKUSAIDIA KUONGEZA NGUVU YA KUOMBA

Kuna mambo mengi sana yanayoweza kukusaidia ili nguvu yako ya maombi na kujibiwa kuongezeka. Tuangalie haya mambo 12:

1. TOBA NA UTAKASO: Kabla ya kuanza kuomba, omba toba kwa ajili yako na yule unayemuombea, jisafishe kwa Damu ya Yesu Kristo, na pia takasa eneo ambalo unaomba na kulikomboa katika ulimwengu wa roho. Nguvu yako ya kuomba inaweza kutegemea eneo ulipo. Hujawahi kuona kuna maeneo unaweza kuomba vizuri lakini kuna maeneo mengine ukishaenda nguvu ya kuomba haipo. Wengine akiwa kwenye kikundi cha maombi kanisani anakuwa na nguvu sana ya kuomba lakini akishafika nyumbani, nguvu yote inaisha. Unadhani shida ipo wapi? Eneo ni muhimu sana katika ulimwengu wa roho.

2. IJUE MAANA YA KUOMBA: Kuomba ni njia mojawapo ya kuzungumza na Mungu wetu. Unapomuita Mungu kwa kuomba anakusikiliza (Yeremia 29:12). “BWANA yu karibu kwa wote wamwitao, Wote wamwitao kwa uaminifu”(Zaburi 145:18). Na njia mojawapo ya kumwita Mungu ni kwa njia ya maombi. “Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua”(Yeremia 33:3). Neno “mambo usiyoyajua” tukiliangalia kwa undani tunaona ni “mafunuo ya Mungu.” Kwa hiyo kuomba kunamfanya Mungu akupe mafunuo(revelation). Hivyo dumu katika kuomba (Wakolosai 4:2) kwani maombi ya mwenye haki yana nguvu (Yakobo 5:16).

3. MUDA: Muda/wakati ni muhimu sana katika ulimwengu wa roho hasa katika kuomba. Waefeso 5:16 inasema “tuukomboe wakati.” Maana yake wakati umetekwa na ibilisi. Moja ya silaha ambazo shetani anatumia kuua maombi ni kutumia muda. Akiweza kuuteka muda wako ameuwa maombi yako. Shetani alitumia sheria kujaribu kufunga muda wa maombi kwa kina Daniel siku 30 (Daniel 4). Kwa kuwa sheria sasa imeandikwa katika mioyo yetu Waebrania 10:16), muda unafungwa katika ulimwengu wa roho na matokeo yanatokea katika mwili.

Kuna watu ambao katika ulimwengu wa roho, shetani amefunga muda wao labda masaa 23 kwa siku. Maana yake katika siku huwezi kufanya maombi zaidi ya saa moja. Pia wengine muda wao umefungwa masaa 23 na dakika 45. Maana yake huwezi kuomba effectively zaidi ya dakika 15. Dakika 15 za mwanzo utaomba vizuri ila zikianza kuzidi, utaanza kupata uzito wa ajabu. Na kuna watu muda wao wa kuomba umefungwa masaa 24 kwa siku. Kwa huyu mtu hata kuomba dakika 5 ni kazi na ukianza tu kuomba, hapo hapo unaanza kusikia uzito. Kumbuka muda unafungwa katika ulimwengu wa roho, hivyo ukitaka kuukomboa, lazima uukomboe katika ulimwengu wa roho.

Na ukianza kufanya maombi ya kukomboa wakati sawa na Waefeso 5:16, shetani atakupiga vita. Lakini unaweza kuanza kukomboa kidogo kidogo. Mfano unashangaa ulikuwa huwezi kuomba nusu saa sasa unaweza. Baadae unaenda unaweza kuomba saa moja na kuendelea. Kama ulikuwa huwezi kuomba hata dakika 5 ni vigumu kuanza ghafla tu uweze kuomba kwa masaa 3 mfululizo. Maombi ya kuukomboa wakati ni maombi ya kufanya mara kwa mara.

4. KUWA NA NENO: Moja ya maombi ambayo yana nguvu sana ni maombi kwa kutumia neno la Mungu kwa imani. Unapokuwa unaomba kutumia neno la Mungu unamkumbusha Mungu kuwa yeye ni nani kwako. Neno la Mungu ni agano amefunga na wewe hivyo ukitumia neno unamkumbusha Mungu juu ya agano alilofunga na wewe. Mfano kama unahitaji uponyaji, unaweza kutumia mistari kama “kwa kupigwa kwake sisi tumepona” (Isaya 53:5) kwa imani. Mistari ya biblia itabaki kama mistari usipopata mafunuo kutoka kwa Roho Mtakatifu.

Unapotoa neno kama hilo kwa imani unampa Mungu kuachilia neno na kukujibu. “Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao” (Zaburi 107:20). Kwa hiyo unapomuomba Mungu kitu fulani hakupi hicho kitu ila anakupa neno lilibeba hicho kitu. Mfano ukiomba uponyaji anakupa neno lilibeba uponyaji na imani yako inakupa kupokea. Ukimuomba hela hakupi hela ila neno ambalo limebeba maarifa ya kupata hela. Ndo maana ni muhimu sana kuwa na neno la Mungu kwani yeye hujibu kwa ufasaha
5. OMBA MUNGU AKUPE MASIKIO YA KUSIKIA: Hiki kipengele kinaweza kuunganishwa na cha 4. Ili maombi yako yakue, unahitaji kuwa na neno la Kristo. Warumi 10:17 inasema “basi imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo.” Kwa hiyo muombe Mungu akupe masikio ya kusikia ili uweze kusikia sauti ya neno lake. Siongelei masikio ya nje bali masikia ya ndani ambayo yanasikia kile ulichosikia. Matayo 13:13 inasema “wakisikia hawasikii wala kuelewa.” Kwa hiyo unaweza kusikia na usisikie kile ulichosikia. Lakini ukimuomba Mungu akupatie masikio ya kusikia itaongeza neno la Mungu ndani yako na kufanya maombi yako yawe na nguvu.

6. JIFUNZE KUUOMBEA MWILI WAKO: Kuomba ni jambo la rohoni na Mungu wetu anapenda tuwe tunaomba. Kwa sababu mwili na roho mara zote vinapingana (Wagalatia 5:17), mwili hautaki kabisa maombi. Kama unabisha siku moja fanya jaribio hili: Andaa maombi ya saa moja halafu mpigie simu rafiki yako mpendwa na umwambie mambo yote unataka kumwambia Mungu. Utakuta unaweza kumwambia rafiki yako kwa muda wa saa moja bila kuchoka. Sasa chukua hayo maombi halafu nenda mbele za Mungu kwa lengo la kuomba, utaona mwili unakugomea. Kwa hiyo ili uweze kuwa na maombi effective, lazima uushinde kwanza mwili.

Maandiko yanasema “Basi ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana” (Warumi 12:1). Kumbuka dunia, mwili, na shetani vinafanya kazi pamoja katika utatu wa uovu kwa ajili ya kupinga chochote kile cha Mungu kama kuomba. Hivyo kuwa na tabia ya kuuombea mwili wako kila siku. Kama unataka kuomba kwa saa moja, omba kwanza na kuukabidhi mwili wako kwa Mungu ili uweze kukubali maombi ya saa moja. Ukianza kuomba utaona mwili unakataa lakini unavyoendelea kuomba, eventually unaushinda na utashangaa unaomba kwa urahisi sana. Uombee mwili wako kila siku.

7. OMBA UPAKO WA KUOMBA: Maandiko yanasema Roho Mtakatifu ndiye anatusaidia kuomba (Warumi 8:26). Hivyo kila siku muombe Roho Mtakatifu akupe upako wa kukusaidia kuomba unapoanza kuomba. Hii ni sala ambayo unatakiwa uifanye kila siku kwani unahitaji Roho wa Mungu akusaidie katika maombi yako yote. Lakini unapoomba upako wa kuomba, muombe Roho Mtakatifu akuongoze kuomba katika kila kitu ili usiombe kwa tamaa zako, kitu ambacho kinaweza kumfanya Mungu asijibu maombi yako (Yakobo 4:3). Pia muombe Roho Mtakatifu akukumbushe neno (Yohana 14:26) la kukusaidia kuomba. Kumbuka kila unachotaka kufanya cha Mungu, kinahitaji upako wa Mungu. Wapendwa wengine huwa wanashindwa kuomba kutokana na kwamba wanajaribu kutumia nguvu zao kuomba.
8. OMBA KWA IMANI: Hiki ni kipengele muhimu kuliko vyote. Unapokuwa unaomba, weka imani yako kwa Yesu. Wengi wanaweka imani kwenye maombi, kwenye kupokea, kwenye kufunga, au kwenye kujibiwa. Unapoweka imani kwenye maombi halafu Mungu asipojibu, utaanza ku-question maombi yako. Na kama upo kwenye kikundi cha maombi utaanza kujiuliza juu ya hicho kikundi cha maombi na wengine wanaweza kuhama kikundi. Maana yake wanatoa imani ya maombi kwenye kundi moja na kuihamisha kwenye kundi jingine. Hii ni kuwa na “imani kwenye maombi” na siyo “kuomba kwa imani.” Lakini ukiweka imani yako kwa Yesu na usipojibiwaa maombi yako utamuuliza Yesu shida ipo wapi na atakujibu kwa kukupa neno lake. “Kwa sababu hii nawaambia, yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu” (Marko 11:24). Unaweza kutumia msitari huo kumuuliza Mungu kwa nini hujapokea kile umeomba wakati amekuahidi utapokea.

9. ONGEZA NGUVU ITENDAYO KAZI NDANI YAKO: Ukisoma Waefeso 3:20 utaona kitu cha ajabu pale. Mungu anasema “Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuwayazayo, na kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu.” Hapa Mungu anatuambia anajibu zaidi ya tunayoomba lakini pia anasema kwa kadri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu. Hivyo moja ya njia ya kuongeza kujibiwa ni kuongeza nguvu ya Mungu ndani yako. Nguvu inayoongelewa ni upako wa Roho Mtakatifu kwani ndo nguvu pekee ambayo inatenda kazi ndani yetu. Ndo maana kama unataka kuongeza nguvu katika maombi yako huwezi kukwepa kujua aina mbali mbali za upako wa Roho Mtakatifu za kukusaidia wewe.

10. MATEGEMEO: Unapoenda mbele za Mungu kuomba unategema nini? Lazima uwe na mategemeo fulani katika maombi yako. Kama hutegemi chochote kutoka kwa Mungu, kwa nini unaomba? Kuna mambo tunatakiwa kuyategemea tunapokuwa tunaomba lakini kuna mambo hatutakiwi kuyategemea. Tegemeo kubwa juu ya maombi ni kwamba “na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake” (1 Yohana 3:22). Kwa hiyo lazima tuzishike kwanza amri za Mungu. Pia katika maombi utegemee kupata maarifa na roho ya ufaham (Wakolosai 1:9). Kuna mambo mengi zaidi ambayo unaweza kutegemea kwenye maombi. Lakini pia kuna mambo ambayo usiyategemee.

Kwanza usitegemee tu kila kitu kitakuwa rahisi. Omba kwa imani lakini usitegemee kuwa kila kitu kitaenda kirahisi kama unavyotaka wewe. “Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam, mimi Paulo, mara ya kwanza, na mara ya pili, na Shetani akatuzuia” (1 Wathesalonike 2:18). Daniel maombi yake yalizuiliwa siku 21 (Daniel 10:13). Kuna kipindi shetani anaweza kuzuia hivyo lazima ujue kuwa kuna wakati unapoomba unaenda kupambana. Uwe na imani ya kushinda lakini usiende kwa kutegemea kila kitu ni rahisi. Na level fulani ya maombi unatakiwa ku-bypass radar ya shetani. Njia mojawapo ni kunena kwa lugha (1 Wakorintho 14:2).

Pili usitegemee muujiza. Watu wengi wanapenda kuomba wakitegemea muujiza. Maandiko hayasemi tutaishi kwa muujiza bali kwa neno (Matayo 4:4). Sina maana kuwa maombi hayawezi kukuletea muujiza lakini usiwe unaenda mbele za Mungu kuomba kwa mategemeo ya muujiza. Miujiza ipo lakini kumbuka kila muujiza una sababu yake kuwepo na wakati wake kuwepo. Sababu na wakati wa kuwepo muujiza ikiondoka na muujiza huondoka (1 Waflme 17:14). Mungu mwenyewe anajua kipindi unahitaji muujiza. Hivyo mategemeo yako yasiwekwe kwenye muujiza bali yawekwe neno la Mungu. Kikubwa na cha msingi ni kwamba “twaenenda kwa imani, si kwa kuona” (2 Wakorintho 5:7).

11. PIMA NGUVU YA MAOMBI YAKO: Utajuaje kama maombi yako yana nguvu au hayana? Nguvu ya maombi haipimwi kwenye muda ambao unautumia kuomba bali kwenye matunda unayoyapata unapoomba.  Maandiko yanasema “kwa matunda yao mtawatambua” (Matayo 7:16). Kwa lugha nyingine nguvu ya maombi yako inapimwa kwenye ongezeko la imani yako. Maombi yanatakiwa yakuze imani yako kwa Kristo na imani yako inapokua hata kujibiwa kwako na kiwango cha maisha kinaongezeka.

Lakini kumbuka kuwa “tunaishi kwa imani”(Warumi 1:17) na wala “hatuishi kwa maombi.” Jinsi nguvu yako ya maombi inavyongezeka ndivyo kujibiwa kutaongezeka na utaweza kuomba kwa muda mrefu. Ila kumbuka urefu wa maombi siyo nguvu ya maombi. Nguvu ya maombi iliyoko ndani yako siyo nguvu yako ila ni nguvu ya Roho Mtakatifu ifanyayo kazi ndani yako. Unaweza kuomba maombi marefu yasiyo na nguvu na pia unaweza kuomba maombi mafupi yakawa na nguvu. Hii inatege

12. MAOMBI YA KUFUNGA: Kuna level fulani ya maombi ambayo unahitaji kufunga na kuomba. Kuna mambo mengine ambayo Mungu hawezi kufanya mpaka umefunga na kuomba. “Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga” (Matayo 17:21). Maombi ya kufunga ni maombi ambayo yana nguvu sana. Unapofunga unatakiwa uombe Roho Mtakatifu akuongoze mambo gani ufunge. Wengi huwa wanafunga kwa kuunyima mwili chakula na maji. Kwa mfano mtu hali asubuhi mpaka jioni.

Lakini wakati mwingine unatakiwa uinyine nafsi pia na hapa ndo huwa pagumu. Nafsi inalishwa kwa kuhisi, kuona, kusikia, kuonja na kunusa. Kwa wengine kufunga kwenye nafsi ni kugumu zaidi ya kufunga kwa mwili. Kuna watu wengine anaweza kufunga chakula siku mbili bila shida ila hawezi kuacha kutumia simu, kuangalia TV, au kusikia mziki. Wakati mwingine unaweza kufunga kwa ajili ya nafsi pia kwani lengo kubwa la kufunga nikujinyima vile mwili na nafsi inahitaji ili kuilisha roho. Soma Isaya 58 juu ya kufunga. Kuna sababu nyingi mtu anaweza kufunga na chache ni hizi:

Kufunga ili kutafuta msaada na mwongozo wa Mungu (Ezra 8:21—23).

Kufunga ili Mungu asikie maombi kilio na maombi yako (Esther 14:6; Nehemia 1:4—11).

Kufunga ili ushinde majaribu (Matayo 4).

Kufunga ili kuwa na upako wa huduma (Matendo 13:3).

MUHIMU: Maombi ni muhimu sana katika maisha ya kila anayeamini. Lakini usijaribu kuishi kwa maombi ila hakikisha unaishi kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu (Matayo 4:4). Watu wengi wameweka imani yao katika maombi kuliko katika neno. Matokeo yake wanakua katika maombi lakini hawakui katika kumjua Kristo kupitia neno lake.

Maombi yana nafasi yake lakini muhimu zaidi hakikisha una neno ili uweze kujenga imani yako. Ukisoma misingi 12 ya imani utakuta maombi siyo moja ya msingi. Umewahi kujiuliza kwa nini watu wengi wanaweza kuomba kila siku lakini hawawezi kusoma neno kila siku? Umewahi kujiuliza kwa nini watu wengi wakiwa wanaumwa au wanashida kitu cha kwanza watasema ni “ninahitaji maombi.” Ni wachache watasema “ninaumwa ninahitaji neno.” Maandiko yanatuambia Mungu hutuma neno la uponyaji (Zaburi 107:20). Hivyo unavyozidi kuongeza nguvu yako katika kuomba

Ubarikiwe!!

SHARE ZAIDI TAFADHALI

No comments:

Post a Comment